30 Aprili 2022 - 12:47

Mfuko wa Fedha Duniani (IMF) umetahadharisha kuwa, kupanda kwa bei ya chakula na mafuta kutokana na vita vinavyoendelea huko Ukraine kunaweza kusababisha machafuko ya kijamii barani Afrika.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Aghalabu ya nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara tayari zimeathirika na mdororo wa kiuchumi tangu mwaka jana kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 na athari mbaya zitaongezeka kutokana na kupanda kwa bei ya nafaka na mafuta. 

IMF imeeleza kuwa, vita vya Ukraine vimechochea kupanda pakubwa kwa bei ya nishati na bidhaa za chakula, masuala ambayo yanaweza kuathiri hali ya usalama katika jamii, kuzidisha viwango vya umaskini, kushadidisha ukosefu wa usawa wa kipato katika jamii na hata kuibua machafuko ya kijamii. 

Ripoti ya IMF inaeleza kuwa, ukuaji wa pato la taifa katika nchi za Afrika mwaka jana wa 2021 ulikuwa asilimiai 4.5; hata hivyo kiwango hicho kinatazamiwa kupungua na kufikia asilimia 3.8 mwaka huu. 

Abebe Aemro Selassie, Mkuu wa Kitengo cha IMF barani Afrika amesema kuwa, anatiwa wasiwasi na tatahira za kupanda kwa pamoja kwa bei ya nishati na chakula; jambo linalohisiwa zaidi katika nchi nyingi za Kiafrika ambazo si wauzaji wa mafuta au gesi nje ya nchi.

Wakati huo huo, bei za vyakula zilizofuatiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) zimeonyesha kupanda kwa asilimia 12.6 ya bei za bidhaa hizo kati ya mwezi Februar na Machi mwaka huu na hivyo kufikia kiwango cha juu zaidi tangu ufuatiliaji huo uanzishwe mwaka 1990. 

Afrika inategemea asilimia 85 ya ngano kutoka nje, huku wategemezi wakubwa wa ngano hiyo zikiwa ni Tanzania, Ivory Coast, Senegal na Msumbiji. 


342/